Zaidi ya watu 20 wauawa Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18397-zaidi_ya_watu_20_wauawa_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema kuwa, watu wasiopungua 25 wameuawa katika mapigano ya hivi karibuni nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2016 11:45 UTC
  • Licha ya madola ya kigeni kuwa na wanajeshi wao Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini bado machafuko yanaendelea.
    Licha ya madola ya kigeni kuwa na wanajeshi wao Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini bado machafuko yanaendelea.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema kuwa, watu wasiopungua 25 wameuawa katika mapigano ya hivi karibuni nchini humo.

Shirika la habari la AFP limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, maafisa sita wa polisi na wanajeshi wanne wameuawa katika shambulio la kuvizia lililofanywa na watu wenye silaha katika viunga vya mji wa Bambari huku watu wengine 15 wakiuawa katika mapigano yaliyozuka baina ya makundi hasimu mjini humo. Taarifa hizo zimeongeza kuwa, zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Katika siku za hivi karibuni, zimeongezeka lawama za kulalamikia kuweko wanajeshi 13 elfu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na vitendo vyao dhidi ya raia. Wananchi wa nchi hiyo wanalalamika kuwa askari hao wanawanyanyasa raia badala ya kuwalinda.

Vikosi vya Ufaransa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wakati huo huo asasi za kiraia ziliitisha mgomo wa nchi nzima wiki iliyopita ili kushinikiza kuondoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Asasa hizo za kiraia zinasema kuwa, askari hao wa Umoja wa Mataifa ndicho chanzo cha kuendelea machafuko nchini humo.