Kumalizika operesheni ya kikosi cha Sangaris nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18511-kumalizika_operesheni_ya_kikosi_cha_sangaris_nchini_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa amefanya safari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa minajili ya kuhitimisha majukumu ya kikosi cha Sangaris nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 31, 2016 04:26 UTC
  • Kumalizika operesheni ya kikosi cha Sangaris nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa amefanya safari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa minajili ya kuhitimisha majukumu ya kikosi cha Sangaris nchini humo.

Jean Yves Le Drian ameelekea nchini humo kuhitimisha majukumu ya kikosi cha askari wa Ufaransa katika hali ambayo siku mbili zilizopita kwa akali watu 25 waliuawa ndani ya taifa hilo. Machafuko na ukatili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati uliibuka wiki kadhaa zilizopita na umekuwa ukiongezeka siku hadi siku. Hii ni katika hali ambayo Rais Faustin-Archange Touadéra wa nchi hiyo ambaye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miezi sita sasa, alihidi kuwanyang'anya silaha wanamgambo sanjari na kurejesha usalama na amani nchini humo.

Sehemu ya watoto waliobakwa na askari wa Ufaransa Sangaris

Kufuatia kuibuka machafuko hayo rais huyo amewataka wanamgambo na raia kulinda umoja wa kitaifa wa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Kadhalika Rais Faustin-Archange Touadéra ameyataja mapatano ya kitaifa kuwa njia pekee kwa ajili ya kuepukana na machafuko na vita vya ndani vya hivi sasa nchini. Amesema kuwa kuibuka upya wimbi la mapigano ambalo limeendana na kuharibiwa makazi ya raia na kadhalika kuwafanya maelfu ya wananchi kuwa wakimbizi, kutaifanya nchi hiyo kukabiliwa na matatizo makubwa kabla ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

Waasi wa Seleka nchini CAR

Machafuko hayo yameshadidi katika hali ambayo, askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wale wa Ufaransa, wapo nchini humo kwa lengo la kutekeleza operesheni za usalama na kurejesha amani. Weledi wengi wa mambo na makundi ya kiraia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekosoa vikali mienendo ya askari hao kwa kuzembea katika utekelezaji wa majukumu yao huku machafuko yakizidi kuongezeka siku hadi siku. Operesheni za askari wa Ufaransa nchini humo zilizopewa jina la Sangaris zinafikia tamati katika hali ambayo kwa mujibu wa wataalamu wa mambo, machafuko yamezidi kushika kasi zaidi. Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alidai kuwa, operesheni za askari wa nchi yake zilifanyika kwa mafanikio na kwamba sasa umefika muda kwa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA kuchukua nafasi yao. Mwaka 2013, serikali ya Ufaransa ilituma sehemu ya askari wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kile ilichokidai kuwa ni msaada wa utatuzi wa kisiasa na kijeshi wa mgogoro wa taifa hilo ambapo mwaka uliopita na baada ya kufanyika uchaguzi na kupatikana usalama wa kiwango fulani, baadhi ya askari hao wa Ufaransa waliondoka nchini humo na kurejea kwao. Hata hivyo zaidi ya askari wengine 2000 waliendelea kusalia nchini humo chini ya mwavuli wa operesheni za Sangaris. Suala muhimu ni hili kwamba uepo wa askari wa Ufaransa katika nchi nyingi za Kiafrika daima umekuwa ni kwa ajili ya kulinda maslahi ya kikoloni ya Paris kinyume na maslahi ya nchi husika.

Magaidi wa Kikristo wa Anti-Balaka Jamhuri ya Afrika ya Kati

Ufaransa ambayo kwa karne kadhaa ilizikoloni nchi nyingi za Kiafrika, hivi sasa pia inajaribu kupenyeza katika baadhi ya nchi hizo kwa madai ya kurejesha usalama na amani katika nchi hizo. Licha ya kwamba operesheni za Sangaris zinamalizika leo, lakini karibu askari 350 wa Ufaransa kikiwemo kikosi kilichojizatiti kwa ndege zisizokuwa na rubani wataendelea kusalia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wakishirikiana na askari wa Umoja wa Mataifa wapatao elfu 10. Kufichuliwa kesi za ubakaji zilizowahusisha askari wa Ufaransa dhidi ya watoto wadogo wa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika katika miezi kadhaa iliyopita, kuliibua wimbi la malalamiko makali nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa, mwezi Disemba mwaka 2013 na mwezi Juni mwaka 2014 askari wa Ufaransa waliwabaka watoto wadogo baada ya kuwarubuni kwa pesa na chakula. Hii ni katika hali ambayo hadi sasa mahakama ya kuwawajibisha askari waliohusika na kashfa hiyo, bado haijaundwa. Hivi sasa raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanatazamia kwamba, kuondoka askari hao wa kigeni nchini kwao kutatoa fursa kwa serikali na bunge la nchi hiyo kuweza kuzuia machafuko na kurejesha usalama na amani nchini.