Kumalizika rasmi muda wa kuhudumu wanajeshi wa Ufaransa nchini CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18589-kumalizika_rasmi_muda_wa_kuhudumu_wanajeshi_wa_ufaransa_nchini_car
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa ametangaza kumalizika rasmi muda wa kuhudumu wanajeshi wa nchi hiyo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2016 04:23 UTC
  • Kumalizika rasmi muda  wa kuhudumu wanajeshi wa Ufaransa nchini CAR

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa ametangaza kumalizika rasmi muda wa kuhudumu wanajeshi wa nchi hiyo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Jean-Yves Le Drian alisema jana katika sherehe zilizofanyika kwa mnasaba huo huko Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuhudhuriwa na maafisa wa ndani na wanadiplomasia wa nchi za kigeni kuwa, muda wa kuhudumu wanajeshi wa kulinda amani wa Ufaransa walioko katika kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati umemalizika.

Jean- Yves Le Drian aliwahi kusema akiwa katika bunge la Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa, kumalizika muda wa kuhudumu walinda amani wa Ufaransa katika nchi hiyo haimaanishi kumalizka uhusiano wa kijeshi kati ya Paris na Bangui. Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa ameongeza kusema kuwa, ingawa jeshi la nchi hiyo litashuhudiwa mara chache huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini jeshi hilo litaendelea kuwajibika nchini humo.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa  jana pia alikuwa na mazungumzo na Rais Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye aliingia madarakani hivi karibuni na kumuahidi rais huyo kuwa Ufaransa itabakisha nchini humo wanajeshi wake 350. 

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadera

Maelfu ya watu wameuawa na wengine milioni nne na laki tano wamekuwa wakimbizi tangu kuzuka mapigano na ukosefu wa amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2013.