5 wauawa katika hujuma dhidi ya msafara wa waziri DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19426-5_wauawa_katika_hujuma_dhidi_ya_msafara_wa_waziri_drc
Kwa akali watu watano wameuawa katika shambulio lililolenga msafara wa waziri katika mkoa wa Kivu Kusini, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2016 04:26 UTC
  • 5 wauawa katika hujuma dhidi ya msafara wa waziri DRC

Kwa akali watu watano wameuawa katika shambulio lililolenga msafara wa waziri katika mkoa wa Kivu Kusini, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Agnes Sadiki, Waziri wa Uchukuzi wa mkoa huo na pia msemaji wa serikali amethibitisha kutokea mauaji hayo na kusema kuwa, watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliushambulia msafara wa Etshiba Mboko, Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa huo ambaye alikuwa akitoka katika mazishi ya nduguye hapo jana.

Sadiki ameongeza kuwa, ingawaje waziri huyo ameponea chupuchupu bila kujeruhiwa katika hujuma hiyo iliyotokea katika kijiji cha Pemba, lakini walinzi wake wawili na watu watatu wa familia yake wameuawa.

Waasi wa DRC ambao wanatekeleza mashambulizi ya mara kwa mara

Hujuma hiyo ya Kivu Kusini imefanyika katika hali ambayo, ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliotumwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutathmini hali ya kisiasa na kiusalama nchini humo, ulikuwa unautembelea mkoa jirani wa Kivu Kaskazini.

Mikoa hiyo miwili imekuwa ikishuhudia mapigano ya kikabila na machafuko ya mara kwa mara, tangu vimalizike vita vya ndani nchini Kongo DR vya kati ya mwaka 1998 na 2003.