UN: Watu milioni 14 watahitajia msaada wa dharura Nigeria 2017
Umoja wa Mataifa umesema watu milioni 14 watahitajia msaada wa dharura mwaka ujao wa 2017 kaskazini mwa Nigeria na kwamba makumi ya maelfu ya watoto wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa katika eneo hilo ambalo lilikuwa ngome ya kundi la wanamgambo wa Boko Haram.
Peter Lundberg, Mshirikishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada ya binadamu nchini Nigeria amesema watu milioni 26 nchini humo wataathirika na migogoro inayolikabili eneo hilo na kwamba milioni 14 miongoni mwao watahitaji msaada wa dharura.
Ofisa huyo wa UN ameongeza kuwa, watoto 75 elfu yumkini watapoteza maisha katika miezi kadhaa ijayo kaskazini mwa Nigeria kutokana na njaa, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.

Mwezi Julai mwaka huu, Manuel Fontaine, Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la Magharibi mwa Afrika alisema kwa jinsi mambo yalivyo hivi sasa na iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, karibuni hivi, kwa wastani watoto 134 wataanza kufariki dunia kila siku kutokana na utapiamlo, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Alizitaka nchi wafadhili kujitokeza katika kufanikisha mpango wa kuyanusuru maisha ya watoto hao na haswa watoto robo milioni ambao wanakabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu katika eneo la Borno, ambalo lilikuwa ngome ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.
Watoto zaidi ya laki nne wenye chini ya umri wa miaka 5 wanakabiliwa na utapiamlo katika majimbo matatu yaliyoko katika eneo la kaskazini mwa Nigeria, ambayo yamekuwa yakishuhudia harakati za Boko Haram.