Nov 27, 2016 07:32 UTC
  • Polisi: Watu 14 wameuawa katika mapigano magharibi mwa Uganda

Polisi ya Uganda imetangaza kuwa, watu wasiopungua 14 wameuawa magharibi mwa nchi hiyo, katika mapigano kati ya polisi na watu wenye silaha.

Lydia Tumushabe, msemaji wa polisi katika mkoa wa Rwenzururu wa magharibi mwa Uganda ametangaza kuwa, watu hao wameuawa katika kipindi cha siku tatu kufuatia mapigano baina ya kikosi cha polisi na watu wenye silaha katika eneo moja kwenye mkoa huo ulioko mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya msemaji huyo wa polisi imesema kuwa, kati ya waliouawa wamo maafisa wawili wa polisi na kwamba, polisi wengine watano wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Lydia Tumushabe, msemaji wa polisi katika mkoa wa Rwenzururu, Uganda

Bi Lydia Tumushabe, msemaji wa polisi katika mkoa wa Rwenzururu wa magharibi mwa Uganda ameongeza kuwa, Alkhamisi iliyopita watu wanne waliokuwa na silaha waliuawa baada ya kushambulia kituo kimoja cha upekuzi.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, wafanya mashambulio hayo ni wafuasi wa ufalme ambao wanataka eneo la Rwenzururu lijitenge na kuwa na mamlaka yake.

Vikosi vya usalama vimepelekwa katika maeneo ya Rwenzururu lililoko katika milima ya Rwenzori na kuimarisha usalama katika maeneo yote ya mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na shambulio lolote tarajiwa kutoka kwa kundi lolote.

Tags