Nov 30, 2016 16:26 UTC
  • Wanamgambo Somalia wawachinja wazee wa vijiji wa Kisuni

Wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia wameuawa kwa kukatwa vichwa na kundi moja la wanamgambo eti kwa kukataa kulipa kodi.

Nur Abdullahi, mmoja wa wazee walionusurika kuuawa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo hao wakufurishaji waliwachinja wazee wanane wanaosimamia vijiji vya jimbo la Galmudug kwa madai ya kukataa kulipa 'zaka' na 'kodi' walizowataka walipe.

Ameongeza kuwa, watu wengine saba wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na wanamgambo hao katika makabiliano hayo ya siku tatu zilizopita, ambapo wanamgambo wenye mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab walivamia vijiji vitano vya eneo hilo na kuanza kuwashurutisha wakazi wake walipe kodi. Habari zaidi zinasema kuwa, wanachama 10 wa kundi hilo la wanamgambo wameuawa katika mapigano hayo ya siku za Jumatatu na Jumanne.

Ukatili wa magenge ya kigaidi Somalia

Abdi Hussein Mohamed, Naibu Gavana wa eneo la Mudug jimbo la Galmudug amesema kuwa, wakazi wa eneo hilo wanapitia kipindi kigumu cha ukame na baa la njaa na hivyo aghlabu yao hawawezi kulipa 'zaka' wanazoshurutishwa kuzitoa na wanamgambo hao.

Mapema mwezi huu wa Novemba, watu karibu 30 waliuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa huko Galkayo, katika mapigano mapya yaliyozuka kati ya vikosi vya majimbo hayo mawili hasimu yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia ya Galmudug na Puntland, licha ya kuweko makubaliano ya usitishaji mapigano.

Kabla ya hapo, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia na mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo Michael Keating, walitoa taarifa mjini Mogadishu ya kupongeza makubaliano yaliyosainiwa baina ya Rais wa Jimbo la Puntland Abdiweli Mohamed Ali Gaas na mwenzake wa Galmudug Abdikarim Hussein Guled ya kumaliza mgogoro na machafuko katika eneo la Galkayo.

 

Tags