Dec 02, 2016 07:41 UTC
  • Watu wanane wauawa katika mapigano nchini Libya

Kwa akali watu wanane wameripotiwa kuuawa katika mapigano mapya yaliyotokea katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Shirika la habari la serikali ya Libya LANA limeripoti kuwa, waasi wanane wameuawa katika mapigano kati ya makundi mawili hasimu ya wabeba silaha, moja likiwa na makao jijini Tripoli na jingine likitokea mji wa Misrata, magharibi mwa nchi.

Inaarifiwa kuwa, makundi hayo mawili ya waasi ya Libya yanazozania udhibiti wa mji mkuu Tripoli.

Hali tete ya kiusalama nchini Libya

Mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini Libya ulianza baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 na mbali na mgogoro huo, nchi hiyo inashuhudia harakati za makundi mbalimbali yenye silaha likiwemo kundi la kigaidi la Daesh.

Mwezi uliopita, Kamati Kuu ya Umoja wa Afrika ilisema baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za bara hilo uliojadili mgogoro wa Libya mjini Addis Ababa, kuwa, mchakato wa kisiasa nchini Libya umekwama na kwamba raia ndio wanaopata madhara zaidi kutokana na hali hiyo isiyofaaa. 

Tags