'Sudan inaiuzia Saudia habari za kipelelezi kuhusu Hizbullah'
Gazeti la al Akbar la Lebanon limeripoti kuwa, serikali ya Sudan inaiuzia Saudi Arabia habari za kipelelezi kuhusu mbinu zinazotumiwa na Hizbullah katika masuala mbalimbali hususan mbinu za harakati hiyo ya Kiislamu za kupambana na utawala ghasibu wa Israel.
Gazeti hilo limeripoti kuwa, miongoni mwa habari za kipelelezi zilizouzwa na serikali ya Sudan kwa Saudia ni kuhusu mbinu zilizokuwa zikitumiwa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika kuwapelekea silaha na zana za kijeshi wapigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza kupitia ardhi ya Sudan.
Habari zinasema ripoti hizo za kipelelezi zinatumiwa na Saudi Arabia na washirika wake kama Marekani na Israel kwa ajili ya kuibana zaidi Hizbullah na kupanga mikakati ya kuwawekea vikwazo watu wanaoshirikiana na harakati huyo. Ripoti zinasema kuwa watawala wa Saudi Arabia watawasilisha faili la Hizbullah katika mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliopangwa kufanyika Aprili mwaka huu kwa lengo la kuilaani harakati hiyo.
Serikali ya Sudan chini ya uongozi wa Rais Omar al Bashir imejiunga na Saudi Arabia katika vita vyake dhidi ya Waislamu wa Yemen kwa kutuma askari wa nchi hiyo kupigana bega kwa bega na Wasaudia na imejiondoa katika kambi ya nchi zinazopinga utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na misaada ya mabilioni ya dola inayopewa na watawala wa kifalme wa Riyadh. Sudan pia imeonesha nia ya kuanzisha uhusiano na utawala katili wa Israel unaoendelea kukalia kwa mabavu kibla cha kwanza cha Waislamu na kuuawa wananchi wasio na hatia wa Palestina.