Dec 10, 2016 13:57 UTC
  • Waasi wa FRPI wa Ituri, nchini Kongo DR
    Waasi wa FRPI wa Ituri, nchini Kongo DR

Mwanajeshi mmoja wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameuawa katika mapigano na waasi wanaojulikana kwa jina la kikosi cha wamapambano wa mkoa wa Ituri FRPI huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika. Waasi hao wanadai wameua na kuteka wanajeshi kadhaa.

Kamanda wa Pili wa kikosi cha operesheni cha jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mkoani Ituri ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mapigano hayo yametokea katika kijiji cha Kabona mkoani Ituri na waasi wamefanikiwa kuua mwanajeshi mmoja wa serikali na kumjeruhi mwengine mmoja.

Mashuhuda wamesema kuwa,waasi hao wametumia silaha nzito kushambulia maeneo ya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hata hivyo wanajeshi hao wamefanikiwa kuzima shambulio hilo la waasi.

Askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika doria

 

Duru zilizo karibu na waasi wa FRPI nazo zimethibitisha kutokea shambulio hilo na kusema kuwa, baadhi ya wanajeshi akiwemo afisa mmoja wa kijeshi wametekwa nyara na waasi hao.

Hata hivyo, Chiko Tshitambwe, afisa msimamizi wa operesheni za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amedai kuwa wanajeshi wa serikali wamefanikiwa kuvunja shambulio hilo la waasi na kuwafurusha.

Tags