Muhula wa Rais Kabila DRC wamalizika, serikali yazima mitandao ya kijamii
Katika hali ambayo muhula wa kisheria wa kuwa uongozini Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaelekea kumalizika, serikali ya Kinshasa imeagiza kukatwa mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, taharuki imetanda katika nchi hiyo, huku serikali ya Kinshasa ikiliagiza Shirika la Mawasiliano kukata mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp, Twitter na Skype kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Jumapili.
Mamlaka ya Posta na Kudhibiti Mawasiliano nchini Kongo (ARPTC) imesema kuwa, wananchi wataweza kutumiana tu jumbe za maandishi lakini jumbe zote za picha na video zitazuiwa baada kuanza kutekelezwa agizo hilo kuanzia Jumapili.
Hii ni katika hali ambayo, polisi ya Kongo DR imetahadharisha kuwa itasambaratisha maandamano na mkusanyiko wowote katika mji mkuu Kinshasa.
Kulingana na uamuzi uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kitaifa kati ya chama tawala na baadhi ya vyama vya upinzani, uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwaka 2018.
Hata hivyo muungano mkuu wa upinzani unasema kuwa, Rais Kabila kama walivyo baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika, anadhamiria kung'ang'ania hatamu za uongozi hatua ambayo ni kinyume na katiba na misingi ya demokrasia.
Duru mpya ya mazungumzo kati ya serikali na wapinzani inaendelea nchini DRC, ingawaje wadadisi wa mambo wameashiria kuwa yumkini yasizae matunda.