Tahadhari ya maafisa usalama wa Tunisia kuhusu kurejea magaidi nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22192-tahadhari_ya_maafisa_usalama_wa_tunisia_kuhusu_kurejea_magaidi_nchini_humo
Licha ya kupita miaka sita ya tangu kutokea mapinduzi ya wananchi huko Tunisia, hali ya usalama ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika bado si ya utulivu na hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa wa kurejea magaidi na kufanya vitendo vya kigaidi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 27, 2016 01:11 UTC
  • Tahadhari ya maafisa usalama wa Tunisia kuhusu kurejea magaidi nchini humo

Licha ya kupita miaka sita ya tangu kutokea mapinduzi ya wananchi huko Tunisia, hali ya usalama ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika bado si ya utulivu na hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa wa kurejea magaidi na kufanya vitendo vya kigaidi nchini humo.

Maafisa usalama wa Tunisia wamewatahadharisha viongozi na wananchi wa nchi hiyo kuchukua hatua za ziada za kukabiliana na misimamo mikali ili kuzuia vijana wa nchi hiyo kujiunga na makundi ya kigaidi ya nje ya Tunisia. Hali ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo imepelekea mamia ya raia wa Tunisia kujiunga na magenge ya kigaidi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama na amani ya nchi hiyo wakati wanaporejea nchini humo. 

Taarifa zilizotolewa zinaonesha kuwa, vijana wengi wa kike na wa kiume wa Tunisia wamekuwa wakijiunga na makundi ya kigaidi kutokana na umaskini na ukosefu mkubwa wa kazi nchini mwao. Wengi wa vijana hao wamekuwa wakitumikia makundi ya kigaidi katika nchi za Syria na Iraq. 

Wanamgambo wa Daesh (ISIS)

 

Maelfu ya raia wa Tunisia wamejiunga na kundi la Daesh tangu vilipoanza vita nchini Syria na kufanya mauaji na jinai kubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni, magenge ya kigaidi yamepata pigo kubwa katika nchi za Syria na Iraq na hali hiyo imewalazimisha vijana wa nchi mbalimbali wakiwemo wa Tunisia kuondoka katika nchi hizo na kuanza kurejea walikotoka wakiwa wamepata mafunzo mbalimbali ya kigaidi. Jambo hilo limezusha hofu kubwa kwa wananchi na viongozi wa Tunisia.

Umoja wa Taifa wa Vikosi vya Usalama wa Ndani vya Tunisia umetoa tamko ukisema kuwa, ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa kurejea magaidi nchini Tunisia na kuna hatari ya kuigeuza nchi hiyo kuwa Somalia nyingine. Tamko hilo limeongeza kuwa, wanamgambo hao huwa wanarejea Tunisia wakiwa wamepata mafunzo ya kijeshi na utaalamu wa kutumia silaha za kila namna za kisasa. Indhari hiyo imetolea siku moja tangu viongozi wa Tunisia kutangaza kuwatia mbaroni watu watatu akiwemo jamaa wa Anis Amri, mtuhumiwa wa shambulio la kikatili la wiki iliyopita katika soko moja mjini Berlin Ujerumaini.

 

Hivi karibuni mamia ya watu walikusanyika mbele ya Bunge la Tunisia kulalamikia ruhusa ya kurejea nchini humo, watu wenye misimamo mikali. Kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa mwaka 2015 na Bunge la Tunisia, watu waliojiunga na magenge ya kigaidi nje ya Tunisia, wana haki ya kurejea nchini humo kama raia. 

Siku chache zilizopita, Hadi El Mecdub, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia alisema mbele ya Bunge la nchi hiyo kwamba kuna raia 800 wa Tunisia waliorejea nchini humo baada ya kujiunga na magenge ya kigaidi nje ya Tunisia. Magaidi hao wanavuuka kimagendo katika mpaka wa Tunisia na Libya. Hii ni katika hali ambayo mamia ya magaidi waliorejea Tunisia kutoka katika nchi zenye migogoro na vita vya ndani, hadi hivi sasa wanatembea kwa uhuru nchini humo bila ya kufuatiliwa na sheria. Tena katika hali ambayo nchi jirani ya Libya imo kwenye machafuko na haina utulivu wa kisiasa, suala ambalo limewawepeseshea magaidi kutembea baina ya nchi hizo mbili kwa urahisi mkubwa.

Matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa kazi bado ni mkubwa na kila leo unaongezeka nchini Tunisia. Licha ya juhudi mbalimbali za kuvutia uwekezaji wa kigeni lakini juhudi hizo za viongozi wa Tunisia zimeshindwa kuleta matunda yanayotakiwa. Inavyoonekana ni kuwa, viongozi wa Tunisia wanafanya kila wawezalo kustawisha hali ya kiuchumi na kulinda usalama wa mipaka yao ili kupunguza hatari ya vitendo vya kigaidi nchini humo.