Serikali ya Sudan yawaachilia huru wapinzani kadhaa wa kisiasa
Wapinzani kadhaa wa kisiasa nchini Sudan wameachiliwa huru baada ya kushikiliwa na vyombo vya usalama kwa karibu miezi miwili kufuatia kile kilichoelezwa kuwa nia yao ya kutaka kufanya maandamano dhidi ya serikali.
Mohamed Hassan Arabi msemaji wa Sudanese Congress Party amesema kuwa, wapinzani 20 wa kisiasa ambao takribani miezi miwili iliyopita walitiwa mbaroni na vyombo vya usalama kwa madai ya kutaka kufanya maandamano kulalamikia kupanda kwa bei ya mafuta, waliachiliwa huru jana Jumatatu.
Msemaji huyo wa chama cha upinzani amesema kuwa, bado kuna viongozi wawili wa upinzani wanaoendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Sudan. Mohamed Arabi amesema kuwa, viongozi hao wa upinzani ambao wangali wanashikiliwa ni kiongozi wa chama chao cha Sudanese Congress Party Omer al-Digair na naibu wake Khaled Omer Youssef.
Mwezi uliopita vyombo vya usalama vya Sudan viliwatia mbaroni viongozi kadhaa wa upinzani kwa hofu kwamba, wangefanya maandamano ya kulalamikia kupandishwa kwa asilimia 30 bei ya nishati ya mafuta.
Hayo yanajiri huku Sudan ikishuhudia migomo na maandamano dhidi ya serikali ya Rais Omar al-Bashir. Maandamano hayo yameshika kasi zaidi baada ya serikali ya Khartoum kufuta ruzuku ya wananchi katika sekta ya nishati, suala ambalo limesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu sambamba na ughali mkubwa wa maisha.