Wakimbizi waliorejeshwa Somalia wataka kurejea Dadaab
Akthari ya wakimbizi wa Kisomali waliorejeshwa kwa khiari nchini Somalia wamesema ahadi walizopewa kabla ya kurejeshwa nchini humo hazijatekelezwa na sasa baadhi yao wanataka kurejea katika kambi ya Dadaab nchini Kenya.
Wakimbizi hao wamesema wanajuta kurejea nyumbani kwa kuwa hali ya usalama haijaimarika kama walivyoambiwa na kwamba wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wangali wanafanya mashambulizi ya hapa na pale.
Madino Dhurow, mmoja wa wakimbizi hao ameliambia shirika la habari la News 24 la Afrika Kusini kuwa, yeye pamoja na watoto wake sita hawapati mahitaji na huduma za kimsingi za kila siku kama maji, chakula na matibabu wakiwa katika kambi ya Mogadishu ambako walipokelewa waliporejea Somalia, wakitokea Dadaab ambako wameishi kwa miaka 12.
Wakimbizi hao wanasema jamii ya kimataifa imewatelekeza kwa kuwa hawajapata msaada wowote mwingine, tangu walipopokea dola 400 kwa kila familia kutoka Umoja wa Mataifa, mara tu waliporejea nchini kwao.
Hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilisema kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 hadi sasa, wakimbizi zaidi ya 35,000 wa Somalia wamerejeshwa kwa hiari katika nchi yao kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab.
Miezi kadhaa iliyopita serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuifunga kambi ya Dadaab kikamilifu kufikia mwezi Mei mwaka 2017 kutokana na sababu za kiusalama, kijamii na kiuchumi.