Wabunge Sudan warejesha nafasi ya waziri mkuu
Wabunge nchini Sudan wamepiga kura ya kubadilisha katiba ili nafasi ya waziri mkuu irejeshwa tena nchini humo baada ya miongo miwili.
Rais Omar al Bashir alifuta nafasi ya waziri mkuu baada ya kunyakua madaraka mwaka 1989.
Siku ya Jumatano, wabunge 387 kati ya 425 walipiga kura ya kuunga mkono marekebisho hayo ya katiba ya kuruhusu waziri mkuu ateuliwe na rais na awe na nguvu za utendaji nchini.
Pamoja na hayo, jukumu la kuunda serikali au kuwafuta kazi mawaziri litabakia mikononi mwa rais.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya marekebisho yaliyopendekezwa katika mazugumzo ya kitaifa baina ya serikali na baadhi ya makundi ya upinzani. Mazungumzo hayo yalianza mwezi Oktoba kwa lengo la kusuluhisha matatizo ya kisiasa na kiuchumi na pia kumaliza uasi katika maeneo ya mipakani nchini humo.
Waziri mkuu mpya wa Sudan atakuwa na jukumu la kusimamia serikali hadi wakati wa kufanyika uchaguzi wa bunge mwaka 2020. Tayari Rais Bashir ametangaza kuwa, ataachia madaraka ifikapo mwaka 2020 kwani katiba ya Sudan haitomruhusu kuendelea kutawala.