Mwanadiplomasia wa UN akosoa idadi ndogo ya wanawake katika bunge la Liberia
(last modified Wed, 02 Mar 2016 14:11:31 GMT )
Mar 02, 2016 14:11 UTC
  • Mwanadiplomasia wa UN akosoa idadi ndogo ya wanawake katika bunge la Liberia

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wanawake (UN Women) amekosoa idadi ndogo ya wanawake katika bunge la Liberia na kusema ni muhali kwa sauti za wanawake kusikika vyema kutokana na uwakilishi wao mdogo bungeni.

Phumzile Mlambo-Ngcuka ameashiria idadi ya wanawake kwenye mabunge mawili ya Liberia na kusema asilimia 10 pekee ya wabunge wanawake katika bunge la juu na asilimia 11 katika bunge la chini haitoshi kufikisha kilio cha wanawake katika taasisi za serikali. Bi. Mlambo-Ngcuka amesema kwa kuzingatia kwamba rais wa Liberia ni mwanamke, ilitarajiwa kwamba idadi ya wanawake katika serikali hususan bunge ingekuwa kubwa lakini kwa masikitiko makubwa, nchi hiyo inashikilia nafasi ya 40 kati ya 54 barani Afrika kwa kuwa na idadi ndogo ya wajumbe wanawake. Liberia pia ni ya 113 duniani katika uwanja huo. Sheria ya nchi hiyo inataka uwakilishi wa wanawake uwe wa asilimia 30 katika taasisi za umma lakini sheria hiyo iko kimya kuhusu viti vya kuchaguliwa.

Tags