Watu 37 wauawa katika shambulizi la bomu kaskazini mwa Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23824-watu_37_wauawa_katika_shambulizi_la_bomu_kaskazini_mwa_mali
Makumi ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi la bomu karibu na kambi ya jeshi kaskazini mwa Mali leo Jumatano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 18, 2017 13:09 UTC
  • Watu 37 wauawa katika shambulizi la bomu kaskazini mwa Mali

Makumi ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi la bomu karibu na kambi ya jeshi kaskazini mwa Mali leo Jumatano.

Taarifa ya Jeshi la Mali imesema kuwa, kwa akali watu 37 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa, baada ya gari lililokuwa na mabomu kuripuka nje ya kambi ya jeshi mjini Gao, kaskazini mwa nchi hiyo.

Kader Touré, mkazi wa mji wa Gao amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, yumkini idadi ya waliouawa katika hujuma hiyo ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata makumi ya wahanga wa shambulizi hilo la bomu.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeituhumu serikali ya Mali kuwa imeshindwa kuwadhaminia usalama wananchi na kwamba makundi ya waasi yamekuwa yakitembea huku na kule yakiwahangaisha watu na kuwalazimisha wawakabidhi watoto wao.

Hata hivyo Salif Traore, Waziri wa Usalama wa Mali amekataa kulizungumzia suala hilo akisisitiza kuwa, serikali inafahamu changamoto za kiusalama zilizopo hususan katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo tangu mwaka 2012, lakini inafanya kila liwezekanalo kudhibiti hali hiyo.

Haya yametokea siku mbili baada ya Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa kulitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuwawekea vikwazo wahusika wakuu wa ukiukaji makubaliano ya amani nchini Mali.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyasema hayo juzi katika ripoti iliyosambazwa kwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama na kubainisha kuwa, makubaliano hayo ya amani ya mwaka 2015 kati ya serikali na makundi ya waasi yanatekelezwa kwa mwendo wa kinyonga na hivyo kuna haja ya kuwekewa vikwazo wanaoweka vizingiti kwenye mchakato wa amani nchini Mali.