Serikali ya Sudan yafikia makubaliano ya amani na waasi
Serikali ya Sudan imefikia makubaliano na kundi moja la waasi wa Darfur linalojiita Jeshi la Ukombozi wa Sudan ikiwa ni katika kalibu ya mwafaka wa amani ya Darfur uliotiwa saini mjini Doha Qatar.
Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Musa Muhammad Ahmad, mshauri wa Rais wa Sudan akisema kwenye kikao cha kutia saini makubaliano hayo kuwa, wigo wa makubaliano ya amani nchini Sudan umepanuka zaidi na hivi sasa mantiki ya kufanya mazungumzo inasikika zaidi.
Kwa upande wake, Abul Qasim Imam al Hajj, mkuu wa kundi la waasi wa Jeshi la Ukombozi wa Darfur amesema, "mapinduzi ya pili" ndilo tatizo kubwa katika utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya makundi ya Sudan. Amesema, anataraji kuwa makubaliano hayo yataleta maendeleo na ustawi katika jimbo la Darfur.
Naye Bw. Jeremiah Nyamane Kingsley Mamabolo, mkuu wa opereseheni ya pamoja na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur inayojulikana kwa jina la UNAMID ameyataka makundi yanayokwamisha utekelezaji wa makubaliano ya amani nchini Sudan yajiunge na makubaliano hayo.
Uchumi wa Sudan umeporomoka sana katika miaka ya hivi karibuni huku mapigano na machafuko ya umwagaji wa damu yakiendelea katika majimbo ya Darfur, Blue Nile na Kordofan Kusini.
Mapigano katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan yalianza mwaka 2003 baina ya serikali na makabila ya jimbo hilo.
Hadi hivi sasa watu wanaokadiriwa kufikia laki tatu wamekuwa wahanga wa machafuko hayo na karibu laki tano wengine wamekuwa wakimbizi.