Jan 23, 2017 15:08 UTC
  • Polisi mmoja auawa kaskazini mashariki mwa Kenya

Jeshi la polisi nchini Kenya limetangaza habari ya kuuawa afisa mmoja wa polisi wakati wanamgambo wanaosadikiwa ni wa kundi la kigaidi la al Shabab walipotega mabomu katika benki moja na mikahawa miwli huko Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Shirika la habari la IRNA limezinukuu duru za usalama za Kenya zikitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, kundi la watu wenye silaha lisilojulikana ndilo lililofanya mashambulizi hayo na kupelekea polisi mmoja kuuawa.

Vyombo vya habari vya Kenya navyo vimeripoti habari hiyo na kusema kuwa, muda mchache baada kutokea shambulio hilo, maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya wameimarisha ulinzi katika jengo la tawi la Benki ya Equity ambalo kuta zake zimeharibiwa na vioo vyake kuvunjika.

Baada ya hapo wanajeshi hao waliifunga benki hiyo pamoja na mkahawa na kioski cha chakula kilichoko upande wa pili wa nyumba ya naibu gavana wa Mandera kwa ajili ya kuchunguza iwapo kuna miripuko mengine kwenye eneo hilo au la.

Wananchi wakiwa wamekusanyika mbele ya tawi la Benki ya Equity mjini Mandera baada ya kutokea mripuko wa bomu

 

Kamishna wa Kaunti ya Mandera, Frederick Shisia amesema, afisa huyo wa polisi ameuawa katika shambulio lililofanyika kwenye mkahawa ulioko karibu na nyumba ya naibu gavana wa Mandera.

Amri ya kutotoka nje na kutotembea ovyo imewekwa kuanzia magharibi hadi asubuhi katika Kaunti ya Mandera kufuatia mashambulizi hayo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, vyombo vya usalama vya Mandera vimeanzisha opereseheni maalumu ya kujua ni kundi gani hasa lililohusika na shambulio hilo.

Hata hivyo kidole cha lawama kinaelekezwa kwa kundi la kigaidi la al Shabab la nchini Somalia ambalo lina kawaida ya kufanya mashambulizi ya namna hiyo.

Tags