EU yataka kuachiliwa huru mara moja Sheikh Zakzaky nchini Nigeria
Umoja wa Ulaya umewataka viongozi wa Nigeria kuheshimu amri ya mahakama ya kumwachilia huru mara moja kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.
Mtandao wa habari wa Nation wa nchini Nigeria umemnukuu mwakilishi wa Umoja wa Ulaya mjini Abuja akisema kuwa, umoja huo unasikitishwa na hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuendelea kumshikilia korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuitaka serikali hiyo iheshimu amri ya mahakama ya kumwachilia huru haraka kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Shirikisho la Nigeria hivi karibuni lilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo inavunja waziwazi sheria za kimataifa kwa kukataa kumwachilia huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu.
Siku ya Jumapili, Rais Muhammadu Buhari alitoa matamshi ya kuchekesha akidai kuwa, maslahi ya wananchi hayairuhusu serikali yake kutekeleza amri ya mahakama ya kumwachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Nalo Shirika la Amnesty International juzi Jumatatu lilitoa tamko na kuitaka serikali ya Abuja kumwachilia huru mara moja kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Ofisi ya harakati hiyo iliyoko katika jimbo la Adamawa nayo imesema, kitendo cha serikali ya Rais Muhammadu Buhari cha kukaidi amri ya mahakama na kuendelea kumshikilia Sheikh Ibarahim Zakzaky ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.