Matatizo ya kifedha, changamoto kubwa kwa Umoja wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24423-matatizo_ya_kifedha_changamoto_kubwa_kwa_umoja_wa_afrika
Kuendelea matatizo ya kifedha kwa Umoja wa Afrika (AU) ambayo ndio taasisi kubwa kwa nchi za Kiafrika, kumeufanya umoja huo ushindwe kutekeleza majukumu yake hususan suala zima la kusimamia amani na uthabiti katika eneo hilo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 30, 2017 00:31 UTC
  • Matatizo ya kifedha, changamoto kubwa kwa Umoja wa Afrika

Kuendelea matatizo ya kifedha kwa Umoja wa Afrika (AU) ambayo ndio taasisi kubwa kwa nchi za Kiafrika, kumeufanya umoja huo ushindwe kutekeleza majukumu yake hususan suala zima la kusimamia amani na uthabiti katika eneo hilo.

Erastus Mwencha, Naibu wa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), sanjari na kuonyesha wasi wasi juu ya hali ya kifedha ya AU amesema kuwa, hivi sasa umoja huo unakabiliwa na changamoto kubwa katika kujidhaminia gharama za utendaji kazi wake katika nchi za Kiafrika hususan Somalia. Huku akiashiria kwamba hali hiyo imetokana na kupungua kwa bajeti inayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya, amesema kuwa ni suala la kusikitisha kwamba, UN inaupatia Umoja wa Afrika bajeti ndogo ambayo haiwezi kukidhi mahitaji yake. Ameongeza kuwa, huku hali ikiwa hivyo kwa Umoja wa Mataifa, nao Umoja wa Ulaya umekusudia kupunguza uungaji mkono wake wa kifedha kwa AU.

Erastus Mwencha, Naibu wa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika

Upungufu wa bajeti na kushindwa kutoshelezea miradi ya AU, kunajiri katika hali ambayo hivi sasa umoja huo ambao ndio taasisi kubwa barani Afrika, una nafasi muhimu katika utatuzi wa migogoro mingi ya kieneo kama vile kusimamia operesheni za amani katika eneo hilo. Ushiriki wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Ash-Shabab na kuwekwa katika mipaka ya Somalia askari hao kwa ajili ya kusaidia kurejesha usalama na amani ya nchi hiyo, ni miongoni mwa kazi muhimu zinazofanywa na Umoja huo.

Bendera ya Umoja wa Ulaya

Karibu askari elfu 22 wa Umoja wa Afrika wako nchini Somalia tangu mwaka 2007 kwa lengo la kupambana na wanachama wa kundi la ash-Shabab. Katika hali ambayo usalama umerejea kwa kiasi fulani huku nchi hiyo ikijiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa rais ili kuboresha hali ya kisiasa nchini humo, kukosekana vyanzo vya fedha na uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kuwaondoa askari wake kabla ya muda, kunaweza kusababisha hatari ya kurejea tena ugaidi katika taifa hilo la Pembe ya Afrika. Katika hali ambayo zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Umoja wa Afrika inadhaminiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya, siku chache zilizopita EU ilitangaza kuwa ina mpango wa kupunguza bajeti yake kwa umoja huo kwa asilimia 20. Ukweli ni kwamba tatizo la kudhamini vyanzo vya fedha vya Umoja wa Afrika hivi sasa inahesabiwa kuwa changamoto kubwa kwa taasisi hiyo.

Bendera ya Umoja wa Mataifa

Utegemezi ilionao AU kwa taasisi za kimataifa hususan Umoja wa Ulaya, ambao umeathiri utendaji kazi wa AU, umekuwa na taathira hasi kwa umoja huo. Ni kama ilivyojiri katika kadhia ya Burundi, ambapo kitendo cha Umoja wa Ulaya kukataa kulipa mishahara kwa askari wa kusimamia amani wa nchi hiyo kilichotokana na mashinikizo ya kisiasa kwa Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuliifanya serikali ya Bujumbura itishie kuwaondoa askari wake hao kutoka Somalia. Kwa kuzingatia kuwa vyanzo vya fedha vimekuwa na ulazima kwa ajili ya utendajikazi wa Umoja wa Afrika, ndio maana vinapewa umuhimu mkubwa. Katika fremu hiyo inaonekana kwamba, badala ya nchi wanachama wa AU kuendelea kusubiria misaada ya asasi za kimataifa, zinatakiwa kuangalia upya namna ya kujidhaminia mahitaji yao hayo.

Sehemu ya askari wa Burundi wanaosimamia amani nchini Somalia

Kuainishwa na kuongezwa ada ya haki ya uanachama wa kila mwaka, juhudi kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa eneo na kuongeza uwekezaji kupitia fremu ya kuboresha mazingira ya uchumi wa nchi za eneo na pia kuongeza uwezo wa kifedha, ustawi wa ushirikiano wa kieneo katika fremu tofauti za kisiasa, kiuchumi na kijamii, juhudi kwa ajili ya kuimarisha usalama na uthabiti katika eneo, yote hayo ni katika njia zinazoweza kuimarisha mfumo wa kifedha wa umoja huo suala ambalo kwa sasa ndilo linalohitajika kwa nchi za eneo hilo.