Sudan yakosoa sheria ya kibaguzi ya Trump dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24519-sudan_yakosoa_sheria_ya_kibaguzi_ya_trump_dhidi_ya_waislamu
Msuguano wa kidiplomasia kati ya Washington na Khartoum umeibuka tena baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kupasisha sheria ya kuzuia raia wa Sudan na nchi nyingine 6 za Kiislamu kuingia nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 31, 2017 10:15 UTC
  • Sudan yakosoa sheria ya kibaguzi ya Trump dhidi ya Waislamu

Msuguano wa kidiplomasia kati ya Washington na Khartoum umeibuka tena baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kupasisha sheria ya kuzuia raia wa Sudan na nchi nyingine 6 za Kiislamu kuingia nchini Marekani.

Garibullah Al-Khidir, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan amekosoa vikali sheria hiyo ya kibaguzi na kusema kuwa, uamuzi huo wa Washington umepitwa na wakati  na kuwa utakuwa na taathira hasi kwa uhusiano wa nchi mbili hizo.

Hapo jana Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilimuita balozi mdogo wa Marekani mjini Khartoum, Steven Koutsis, kwenda kujieleza kufuatia hatua ya serikali ya Washington kupasisha sheria hiyo ya kibaguzi dhidi ya nchi hiyo na nyingine sita ambazo aghalabu ya raia wake ni Waislamu.

Kampeni ya kutaka Trump asiingie Uingereza kufuatia sheria yake ya kibaguzi

Hii ni katika hali ambayo, siku chache kabla ya kumaliza hatamu za uongozi wake, rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alitangaza kuiondolea Sudan vikwazo vya kiuchumi vilivyodumu tangu mwaka 1997, ambapo ilitazamiwa kuwa uhusiano wa pande mbili kati ya nchi mbili hizo ungeimarika baada ya kuondolewa vikwazo hivyo. 

Hatua hiyo ya Trump imekosolewa sana na nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa za kutetea haki za binadamu. Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, amri iliyotiwa saini na Rais Donald Trump wa Marekani ya kuzuia raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini Marekani ni kinyume cha sheria za kimataifa. 

Donald Trump, Rais wa Marekani

Mbali na Sudan, nchi nyingine zilizoathiriwa na sheria hiyo ya kibaguzi ya Trump ni Somalia, Syria, Iran, Iraqi, Libya na Yemen.