Algeria yaishitaki Ufaransa kuhusu majaribio ya silaha za nyuklia
Taasisi moja ya kutetea haki za binadamu ya Algeria imeifungulia mashtaka serikali ya Ufaransa kutokana na hasara zilizosababishwa na majaribio ya nyuklia yaliyofanywa na nchi hiyo katika ardhi ya Algeria.
Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Algeria kwa mnasaba wa kutimia miaka 57 tangu Ufaransa ifanye majaribio ya silaha za nyuklia kwenye jangwa la kusini mwa Algeria imesema kuwa: Ufaransa inapaswa kukiri rasmi kuhusu jinai ilizozifanya dhidi ya watu wa Algeria katika kipindi cha ukoloni ikiwa ni pamoja na majaribio yake ya silaha za nyuklia ikishirikiana na Israel na iwalipe Waalgeria hasara za kimaada na kiroho na jinai hizo.
Taasisi hiyo imezitaka pia jumuiya nyingine za kitaifa na kimataifa zifungue mashtaka dhidi ya serikali ya Paris kutokana na hasara kubwa zilizosababisha na majaribio yake ya silaha za nyuklia katika ardhi ya Algeria ambayo yalisababishwa vifo vya maelfu ya Waalgeria.
Mwaka 1960 hadi 1966 Ufaransa ilifanya majaribio 17 ya silaha za nyuklia katika jangwa la Algeria ambayo yaliua karibu watu elfu 42 na kuwasababishia matatizo ya aina mbalimbali maelfu ya wengine. Majaribio hayo ya nyuklia pia yamesababisha hasara kubwa kwa mazingira ya Algeria.