Madaktari wafanya tena mgomo nchini Zimbabwe
Madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya wameanza mgomo wa nchi nzima kushinikiza nyongeza ya mishahara na kuboreshwa mazingira ya kufanyia kazi.
Edgar Munatsi, Rais wa Muungano wa Madaktari Zimbabwe (ZHDA), amesema shughuli zimelemazwa katika hospitali za umma kote nchini kutokana na mgomo huo wa madaktari, akisisitiza kuwa wamelazimika kufanya mgomo kuishinikiza serikali itekeleze matakwa yao.
Amesema mbali na serikali kuwafanyisha kazi kupita kiasi na kusimamisha mpango wa kuwaajiri wahudumu wapya wa afya, pia imekataa kuangalia upya nyongeza ya marupurupu kutoka dola 288 za Marekani hadi 720 kwa mwezi, kwa madaktari wa kiwango cha chini.
Juhudi za David Parirenyatwa, Waziri wa Afya wa Zimbabwe za kuwarai wahudumu hao wa afya warejee kazini huku serikali ikitafuta njia ya kushughulikia maslahi yao, hazijafua dafu.
Mwezi Julai mwaka jana, walimu, madaktari na wauguzi nchini Zimbabawe walifanya mgomo kulalamikia kucheleweshwa mishahara yao.
Hivi karibuni tovuti ya habari ya 'Utafiti na Masoko' ilitoa ripoti iliyoonyesha kuwa pato la wastani la raia wa Zimbabwe ni dola 200 za Marekani na hivyo kuitaja nchi hiyo kuwa nchi masikini zaidi barani Afrika.