UNICEF: Watoto milioni 2 wa Sudan wanakabiliwa na utapiamlo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25216-unicef_watoto_milioni_2_wa_sudan_wanakabiliwa_na_utapiamlo
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema unahitaji dola milioni 110 za Marekani ili kuwanusuru mamia ya maelfu ya watoto ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na utapiamlo nchini Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2017 04:20 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 2 wa Sudan wanakabiliwa na utapiamlo

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema unahitaji dola milioni 110 za Marekani ili kuwanusuru mamia ya maelfu ya watoto ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na utapiamlo nchini Sudan.

Taarifa ya UNICEF imesema kuwa, asilimia 13 ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu wanaishi nchini Sudan na hivyo kuna haja ya kuchukuliwa hatua za dharura ili kuwanusuru.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umesema kuwa, hali hii imewaathiri zaidi watoto katika maeneo ya Darfur, Kordofan Kusini na Kaskazini, Blue Nile na Abyei.

Ramani ya Sudan inayoonyesha maeneo yaliyoathiriwa zaidi na el-Nino

Kadhalika ripoti ya UNICEF imesema kuwa watoto milioni 3 katika maeneo hayo wamelazimika kukatiza masomo kutokana na utapiamlo na lishe duni, vilivyosababishwa na kiangazi, mapigano na mafuriko katika baadhi ya maneo.

Ripoti ya mwezi jana ya shirika la Save The Children ilionyesha kuwa, zaidi ya watoto milioni sita na nusu wa bara la Afrika wanakabiliwa na hatari ya utapiamlo na kufariki dunia, hususan katika nchi masikini na zile zinazokumbwa na ukame kama vile, Somalia, Ethiopia, Sudan na Kenya.

Kwa mujibu wa Save The Children, hali hii imesababishwa na taathira hasi za el-Nino na upungufu wa mvua za kutosha ulioshuhudiwa kwa miaka kadhaa mtawalia katika nchi hizo.