AI: Kufanyike uchunguzi wa mashambulizi ya silaha za kemikali Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26070-ai_kufanyike_uchunguzi_wa_mashambulizi_ya_silaha_za_kemikali_darfur
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na serikali ya Sudan dhidi ya raia katika eneo la Darful lililoko magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2017 12:11 UTC
  • AI: Kufanyike uchunguzi wa mashambulizi ya silaha za kemikali Darfur

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na serikali ya Sudan dhidi ya raia katika eneo la Darful lililoko magharibi mwa nchi hiyo.

Katika ripoti yake mpya, Amnesty International imetaka kufanyike uchunguzi kamili kuhusu mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanyika katika miezi ya Januari hadi Disemba mwaka uliopita wa 2016 katika jimbo la Darfur. 

Taarifa iliyotolewa na maafisa wa Umoja wa Mataifa imeashiria mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la serikali ya Sudan katika eneo la Darfur na kusema kuwa, kushindwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo kunatia aibu na fedheha kubwa.

Katika ripoti yake ya mwezi Septemba mwaka jana, Amnesty International ililituhumu jeshi la Sudan kuwa limetumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake dhidi ya vijiji vya eneo la Jabal Murrah katika eneo la Darfur. Ripoti hiyo ilikadiria kuwa watu baina ya 200 na 250 waliuawa katika mashambulizi hayo ya silaha za kemikali na kwamba wengi wao walikuwa watoto wadogo.

Image Caption

Ripoti hiyo ilikuwa na picha za watoto wadogo walioathiriwa na mashambulizi ya silaha za kemikali ya jeshi la serikali ya Sudan na vilevile picha za satalaiti za vijiji vilivyoharibiwa na mashambulizi hayo.

Rais wa Sudan Omar al Bashir

Itakumbukwa kuwa mwaka 2009 na 2010 Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa waranti wa kutiwa nguvuni Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur.