Kamisheni ya Haki za Binadamu yaikosoa Jordan kwa kumkaribisha al Bashir
Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeikemea serikali ya Jordan kwa kumkaribisha nchini humo Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid bin Ra'ad al-Hussein imesema kuwa, serikali ya Jordan imekiuka majukumu yake ya kimataifa kuhusu watuhumiwa wa kutenda jinai na uhalifu wa kivita kwa kumkaribisha Rais Omar al Bashir wa Sudan nchini humo.
Rais Omar al Bashir wa Sudan alishiriki katika mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliofanyika siku chache zilizopita nchini Jordan.
Kabla ya mkutano huo shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch (HRW) lilitoa wito wa kuzuiwa Rais Omar al Bashir wa Sudan kuingia nchini Jordan.
Katika tamko lake Human Rights Watch ilisema, kwa vile Jordan ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ina wajibu wa kutekeleza makubaliano yaliyounda mahakama hiyo.
Mahakama ya ICC inasema kuwa Rais Omar al Bashir wa Sudan amehusika katika jinai za kivita zilizofanyika kwenye jimbo la Darfur na imetoa waranti wa kutiwa mbaroni kiongozi huyo.
Jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan lilikumbwa na machafuko tangu mwaka 2003 kulalamikia kudharauliwa na kutelekezwa na serikali.