Apr 14, 2017 03:56 UTC
  • UN: Kipindupindu kimeua zaidi ya watu 530 Somalia

Umoja wa Mataifa na jumuiya za misaada ya kibinadamu zimeonya kwamba kipindupindu kinaenea kwa kasi katika maeneo yaliyoathirika na ukame nchini Somalia wakati nchi hiyo ikiendelea kunyemelewa na hatari kubwa ya baa la njaa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa, kesi zaidi 21,000 za kipindupindu zimeripotiwa nchini Somalia na kwamba watu 533 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo huko Somalia tangu mwanzo wa mwaka huu.

Msemaji wa Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Jens Laerke amesema kuwa, mikoa miwili ya Juba ya Kati na Bakool, ndiyo iliyoathiriwa zaidi na ugonjwa huo. 

Watu walioathiriwa na vita, njaa na maradhi, Somalia

Wakati huo huo Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na jumuiya ya Hilali Nyekundu zimetangaza kuwa, ugonjwa wa kipindupindu umeua watu wasiopungua 28 katika eneo lililojitangazia kujitawala la Somaliland katika kipindi cha siku yapata kumi zilizopita na waathitika wengine 170 wanalazwa hospitalini. 

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa, watu milioni 6.2 ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Somalia, wanahitajia msaada wa haraka wa kibinadamu na milioni 2.9 kati yao wanaosumbuliwa na njaa iliyopindukia.

 

Tags