Marekani yalegeza misimamo yake kwa Sudan
Tangu baada ya Rais Omar al Bashir wa Sudan kujiunga na Saudi Arabia katika mashambulizi dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Yemen, nchi za Magharibi zimeonekana kulegeza misimamo yao kuhusu serikali ya Khartoum. Kwa mara ya kwanza Sudan imeruhusiwa kushiriki katika kikao cha wakuu wa kikosi cha pamoja cha kundi la nchi za Marekani, Ulaya na Afrika, maarufu kwa jina la Africom.
Mtandao wa habari wa Middle East Monitor umemnukuu Ahmad Khalifa al Shami, msemaji wa jeshi la Sudan akisema kuwa, kuruhusiwa nchi yake kushiriki katika kikao cha wakuu wa majeshi ya nchi za kundi la Africom linalozishirika nchi za Marekani, Ulaya na Afrika kuna maana kwamba Sudan inaelekea kutolewa katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi na hatimaye kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.
Amesema, kushiriki Sudan kwenye kikao hicho kunaonesha kuwa Khartoum iko tayari kushirikiana na nchi nyingine katika masuala mbalimbali kama vile katika vita dhidi ya uhalifu wa kimataifa, ugaidi, uhamiaji haramu, magendo ya silaha na utakatishaji fedha.
Siku ya Jumapili, Sudan ilitangaza kuwa, tarehe 18 hadi 20 mwezi huu wa Aprili, Luteni Jenerali Imad-Eddin Mustafa Adawi, mkuu wa jeshi la nchi hiyo atakuweko mjini Stuttgart, Ujerumiani kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa kikosi cha Africom kinachoundwa na Marekani, Ulaya na Afrika. Mawaziri wa Ulinzi wa nchi 50 za Afrika nao wanashiriki kwenye kikao hicho.
Mwezi Januari 2017, Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani alifuta vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vya Sudan. Vikwazo hivyo vinasubiri kuondolewa kikamilifu mwezi Juni mwaka huu.
Ikumbukwe pia kuwa, tarehe 7 mwezi huu wa Aprili, Afrika Kusini iliitwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutoa maelezo juu ya kwa nini ilikataa kutekeleza amri ya mahakama hiyo ya kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipoitembelea nchi hiyo miaka miwili iliyopita.