Hatari ya ugaidi, changamoto kubwa zaidi ya Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28518-hatari_ya_ugaidi_changamoto_kubwa_zaidi_ya_misri
Rais Abdulfattah as-Sisi, wa Misri amesema kwamba hatari ya ugaidi ni changamoto kubwa zaidi kati ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2017 23:55 UTC
  • Hujuma ya kigaidi kanisani Misri
    Hujuma ya kigaidi kanisani Misri

Rais Abdulfattah as-Sisi, wa Misri amesema kwamba hatari ya ugaidi ni changamoto kubwa zaidi kati ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Amesema kama zilivyo nchi nyingi za eneo hilo, Misri anakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ameongeza kuwa hakuna njia nyingine ya kukabiliana na tatizo la ugaidi nchini Misri isipokuwa kufanya juhudi za kudumu na za muda mrefu. As-Sisi amesema kuwa Misri ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kutoa onyo kuhusiana na tishio la ugaidi na kuwataka walimwengu wote waungane na kushirikiana kwa ajili ya kuepusha jamii ya mwanadamu na tishio hilo. Amesema vikosi vya jeshi na polisi ya nchi hiyo vinaendesha vita vikali dhidi ya makundi ya kigaidi na ya kuchupa mipaka katika mkoa wa Sinai Kaskazini lakini kwamba pamoja na hali hiyo bado kunahitajika marekebisho makubwa ndani ya nchi hiyo ili kuweza kudhibiti na kuutokomeza kabisa ugaidi.

Rais as-Sisi wa Misri

As-Sisi anatoa matamshi hayo katika hali ambayo Misri katika siku za hivi karibuni imekabiliwa na mashambulio mengi ya makundi ya kigaidi na hasa kutoka magaidi wa Daesh. Siku chache zilizopita milipuko minne ya ugaidi ilitokea katika nchi hiyo ambapo makumi ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Mashambulio kama hayo yangali yanaendelea katika pembe tofauti za nchi hiyo na hasa katika jangwa la Sinai. Hali hiyo imeipelekea serikali ya Cairo kutangaza hali ya hatari nchini na kusisitiza kuendelea kupambana na ugaidi nchini, jambo ambalo limekosolewa na wataalamu wengi wanaosema kuwa hali hiyo haisaidii lolote bali inatumiwa na serikali kuzua hali ya hofu na kukandamiza misingi ya demokrasia nchini. Pamoja na kuwa serikali ya as-Sisi inajaribu kurudisha uthabiti na usalama nchini humo lakini ni wazi kuwa migogoro ya kisiasa na kijamii nchini humo inachochewa na baadhi ya nchi za eneo na Magharibi ambazo zinayafadhili makundi ya kigaidi na hivyo kuimarisha shughuli zao katika ardhi ya Misri. Kupakana kwa nchi hiyo na Libya ambayo usalama wake umevurugika na vilevile Tunisia ni sababu nyingine inayofanya makundi ya kigaidi kujiimarisha huko Misri.

As-Sisi katika safari yake ya hivi karibuni ya kujaribu kuboresha uhusiano na Saudia

Katika upande pili, Misri daima imekuwa ikichukuliwa kuwa ni nchi muhimu na ya kiistratijia katika eneo na hivyo kutazamwa kwa jicho la tamaa na nchi za Magharibi na hasa Marekani. Nchi hizo daima zimekuwa zikifanya juhudi za dhahiri na za nyuma ya pazia ili kuimarisha ushawishi wao nchini humo kwa madhumuni ya kulinda maslahi yao katika eneo. Madai ya kupambana na ugaidi ni kisingizio tu ambacho kimekuwa kikitumiwa na nchi hizo za Magharibi ili kupata fursa ya kujipenyeza na kujiimarisha nchini Misri. Mbali na hayo uhusiano wa Misri na nchi za eneo ni changamoto nyingine inayoikabili serikali ya as-Sisi. Uhusiano mbaya wa Misri na Saudia pamoja na nchi nyingine kadhaa za Ghuba ya Uajemi kuhusu masuala muhimu ya kieneo na kimataifa na hasa kuhusiana na mgogoro wa Syria, umezua mvutano kati ya nchi hizo na kuzipelekea kuunga mkono makundi ya kigaidi yanayoendesha shughuli zao za kigaidi katika ardhi ya Misri.

Mashambulio ya magaidi wa Daesh katika moja ya makanisa ya Misri

Mbali na suala la ugaidi Misri pia inakabiliwa na migogoro mingine ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Licha ya as-Sisi kutoa ahadi chungu nzima za kuimairisha uchumi wa Misri lakini madeni ya ndani na nje yamezidi kurundikana na hivyo kuongeza ughali wa maisha dhidi ya mwananchi wa kawaida wa nchi hiyo. Kuongezeka kiwango cha umasikini na ukosefu wa kazi ni changamoto nyingine inayowakodolea macho viongozi wa serikali ya Cairo, na hivyo kuamsha hasira ya Wamisri. Katika mazingira hayo viongozi hao wanajaribu kutatua matatizo ya ndani na hasa kupambana na tatizo sugu la ugaidi ili wahuishe nafasi ya zamani ya kieneo ya nchi hiyo kongwe ya Kiafrika na Kiarabu.