Wakimbizi wa Sudan wanaishi katika hali mbaya nchini Chad
Mashirika ya misaada yaliyoko nchini Chad yametangaza kuwa, wakimbizi wa Sudan wanaoishi katika kambi nne za wakimibizi nchini Chad wako katika hali mbaya huku watoto wadogo wa wakimbizi wakiteseka kwa lishe duni.
Mtandao wa habari wa Africa Time umeripoti habari hiyo leo na kusema kuwa, mashirika ya misaada yamelaani kutelekezwa watoto hao na kuongeza kuwa, hali hiyo mbaya ya lishe duni imewakumba wakimbizi hao kutokana na kupungua chakula katika miaka ya hivi karibuni katika eneo hilo zima.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika mwezi Disemba 2016, kiwango cha lishe duni mno duniani ni asilimia 18.9.
Kambi ya wakimbizi ya Ouré Cassoni nchini Chad ndiyo kambi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Sudan. Kambi hiyo iko umbali wa kilomita 55 kutoka mjini Amdjarss na umbali wa kilomita 7 kutoka katika mpaka wa Sudan na Chad.
Wakimbizi hao wa Sudan wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Chad kutokana na mapigano ya Darfur yanayoendelea tangu mwaka 2003 hadi hivi sasa.
Mapigano ya Darfur yalizuka baada ya wakazi wa jimbo hilo la magharibi mwa Sudan kuchoshwa na kile wanachosema ni kubaguliwa na serikali kuu ya mjini Khartoum.
Hata nchi ya Chad nayo ina migogoro mingi. Hivi sasa inapambana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram, ina mgogoro wa wakimbizi wa ndani, ukame, lishe duni na matatizo mengine mengi.