Tanzania yakanusha kupendelea upinzani katika uchaguzi wa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31942-tanzania_yakanusha_kupendelea_upinzani_katika_uchaguzi_wa_kenya
Serikali ya Tanzania imekanusha madai ya kuunga mkono muungano wa upinzani nchini Kenya katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 18, 2017 11:31 UTC
  • Tanzania yakanusha kupendelea upinzani katika uchaguzi wa Kenya

Serikali ya Tanzania imekanusha madai ya kuunga mkono muungano wa upinzani nchini Kenya katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8.

Hii ni baada ya kuenea taarifa kuwa, muungano wa upinzani NASA, ambao mgombea wake ni Raila Odinga, umedaiwa kuwa ana mpango wa kuanzisha kituo cha kujumlisha matokeo nchini Tanzania.

Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekanusha madai hayo ikisisitiza kwamba, haiwezi kuruhusu chama chochote cha Kenya kuja kuanzisha kituo cha kujumlisha matokeo ya uchaguzi kwa sababu kufanya hivyo ni kuingilia mambo ya nchi hiyo jirani.

Waziri wa Mambo za Nje wa Ushirikiano wa Mambo ya Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dkt Augustine Mahiga amenukuliwa na gazeti la The Citizen akisema alisikia uvumi kuhusu kituo hicho lakini amesisitiza hakuna chama cha siasa cha Kenya kilichoomba kuanzisha kituo cha kujumlisha matokeo yake na Serikali haitakubali.

Mgombea wa urais wa upinzani Kenya Raila Odinga (kushoto) akiwa na Rais Magufuli wa Tanzania miaka ya nyuma

Dkt Mahiga alisema kwamba wameihakikishia serikali ya Kenya kwamba maneno hayo ni ya uongo na hakuna kitu kama hicho.

Gazeti la Daily Nation Jumatatu iliyopita liliripoti kwamba, Juni 2017 NASA ilitangaza kwamba itaanzisha vituo vitatu maalumu kwa ajili ya kujumlisha kura zake katika nchi ya Kenya, Ujerumani na Tanzania. Odinga amekuwa rafiki mkubwa wa Rais Magufuli na alimuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Gazeti hilo lilibainisha kwamba, Serikali ya Tanzania iliridhia mpango huo wa NASA na kwamba, kituo hicho kitawekwa huko Kigamboni. Pia limeeleza kwamba Odinga alifika Tanzania mwezi Mei kwa ajili ya maandalizi hayo.

Hayo yanajiri baada ya Edward Lowassa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo ambaye alikuwa safarini nchini Kenya hivi karibuni kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa usalama Joseph Nkaissery, kutangaza uungaji mkono wake kwa Rais Kenyatta kwa imani kwamba ndiye mgombea bora katika uchaguzi huo.