Jeshi la Misri laangamiza magaidi 40 katika eneo la Sinai
Jeshi la Misri limefanikiwa kuangamiza makumi ya wanachama wa magenge ya kigaidi, katika operesheni yake yenye lengo la kuwafuta kabisa magaidi wenye misimamo mikali ambao wanaendeleza harakati zao katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.
Duru za kijeshi zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, magaidi 40 wameuawa baada ya vikosi vya usalama vya Misri kushambulia ngome zao katika Peninsula ya Sinai, ndani ya wiki moja iliyopita.
Jumatatu iliyopita, raia 7 wakiwemo watoto wawili waliuawa katika shambulio la bomu la kutegwa garini karibu na mji wa al-Arish, katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa Misri, wiki moja baada ya wanajeshi wasiopungua watano wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuuawa katika mripuko mwingine wa bomu lililotegwa ndani ya gari la deraya, katika mji huo.
Mkoa huo wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Eneo hilo halijawahi kushuhudia utulivu tangu magenge ya kigaidi yaanzishe harakati zao mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani Mohamned Mursi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.