Mke wa Rais wa Zimbabwe ataka Mugabe ataje mrithi wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32338-mke_wa_rais_wa_zimbabwe_ataka_mugabe_ataje_mrithi_wake
Mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amemtaka mumewe aanishe na kumtangaza mrithi wa kiti cha rais nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2017 11:06 UTC
  • Mke wa Rais wa Zimbabwe ataka Mugabe ataje mrithi wake

Mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amemtaka mumewe aanishe na kumtangaza mrithi wa kiti cha rais nchini humo.

Grace Mugabe, amewaambia wanachama wa Tawi la Wanawake la chama tawala ZANU-PF kuwa wakati umefika mumewe yaani Rais Robter Mugabe, atangaze shakhsia atakayerithi mikoba yake ili wafuasi wa chama hicho wamuweke kwenye mizani na wamuunge mkono kwa kishindo.

Grace Mugabe ambaye aliwahi kunukuliwa akisema kuwa, mumewe anaweza kuiongoza Zimbabwe hata akiwa kaburini, amesema chaguo la Rais Mugabe la mrithi wake ndilo litakalokuwa la mwisho na wataliunga mkono.

Mugabe amekuwa akiwapiga kalamu nyekundu wakosoaji wake serikalini na hata kuwatimua ndani ya ZANU-PF wanachama wanaoshinikiza mabadiliko ndani ya chama na kutaka ajiuzulu.

Rais Mugabe na mkewe Grace

Mapema mwezi huu, Rais Mugabe alielekea nchini Singapore kwa ajili ya matibabu, hii ikiwa ni safari yake ya tatu ya kitiba nchini humo mwaka huu.

Mugabe ambaye ameitawala Zimbabwe tokea ijinyakulie uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980, amekuwa akisisitiza kuwa atagombea tena urais katika uchaguzi wa mwaka ujao 2018.

Wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wamekuwa wakishiriki maandamano katika mji mkuu Harare, kulalamikia kile wanachodai kuwa ni njama ya kuiba kura katika uchaguzi ujao wa rais; sambamba na kulalamikia hali ngumu ya maisha na mfumko wa bei za bidhaa.