Kongamano la Kimataifa la Quds laanza nchini Nigeria
Kongamano la Kimataifa la Quds ambalo hufanyika kila mwaka limeanza shughuli zake katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Lengo la kongamano hilo ambalo huandaliwa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ni kuhamasisha na kutangaza uungaji mkono kwa Waislamu wa Palestina, haswa wanaoandamwa na jinai za kila leo za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu.
Kongamano hilo linafanyika wakati huu ambapo jeshi katili la utawala haramu wa Israel limeshadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Quds katika mgogoro wa Msikiti wa al-Aqsa, Kibla cha kwanza cha Waislamu.
Wapalestina zaidi ya 10 wameuawa shahidi na askari wa Kizayuni tangu mgogoro huo uripuke wiki mbili zilizopita, makumi ya wengine wamejuruhiwa na wengine wengi kutiwa mbaroni.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeandaa kongamano hilo katika hali ambayo, muasisi na kiongozi wake Sheikh Ibrahim Zakzaky anaendelea kuzuiliwa chini ya mazingira magumu na vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kwa takriban miezi 19 sasa.
Siku chache zilizopita, harakati hiyo iliitahadharisha serikali kuhusu njama yoyote ya kumuua Sheikh Zakzaky na kushambulia wafuasi wa harakati hiyo. Wimbi la mauaji ya Waislamu hususan wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria lilianza tarehe 13 Disemba mwaka 2015 baada ya jeshi la nchi hiyo kushambulia kituo cha kidini cha Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria na kuua mamia ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky wakiwemo watoto wake watatu.