Wachambuzi: Uchaguzi wa Bunge Senegal uligubikwa na vurugu
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Senegal amesema kuwa, uchaguzi wa Bunge uliofanyika jana nchini humo uliandamana na mapungufu na matatizo mbalimbali.
Francis Capatinde amesema vurugu na ukosefu wa mpangilio uligubika zoezi lote la upigaji kura wa jana na kwamba, hali hiyo imejiri katika hali ambayo kwa kipindi kirefu Senegal imekuwa ikifanya chaguzi katika anga ya kidemokrasia.
Capatinde amesema kuwa, matatizo kama vile dosari za kuwasilisha kadi za kugipia kura na kuchelewesha kwa kiasi kikubwa shughuli ya upigaji kura katika baadhi ya vituo ni miongoni mwa matatizo yaliyoshuhudiwa jana na kwamba baadhi ya makundi yanayomuunga mkono Abdoulaye Wade, rais wa zamani wa Senegal, kwa kushirikiana na kiongozi mmoja wa kambi ya upinzani, wameituhumu serikali ya sasa kwamba ilisababisha matatizo hayo kwa makusudi kwa lengo la kuchakachua matokeo.
Akizungumzia chanzo na sababu za vitendo vya utumiaji mabavu katika zoezi la upigaji kura wa jana amesema kuwa, baadhi ya wapinzani na fikra za waliowengi nchini humo wanaamini kuwa, hatua ya Rais Macky Sall kuendelea kumzuilia jela mwana wa kiume wa Abdoulaye Wade na pia Meya wa jiji la Dakar (Khalifa Sall) imezua mjadala mkubwa wa kisiasa nchini humo na kuwa chanzo cha kuibuka machafuko katika uchaguzi wa jana.
Wapinzani nchini Senegal wanaituhumu seikali ya Rais Macky Sall kwamba, imekuwa ikikandamiza wapinzani.