Rais wa Zambia apongeza kustawi kukubwa uchumi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33810-rais_wa_zambia_apongeza_kustawi_kukubwa_uchumi_wa_iran
Rais Edgar Lungu wa Zambia amepongeza ukuaji wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kuwepo uhusiano mzuri wa pande mbili kati ya Tehran na Lusaka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2017 10:52 UTC
  • Rais wa Zambia apongeza kustawi kukubwa uchumi wa Iran

Rais Edgar Lungu wa Zambia amepongeza ukuaji wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kuwepo uhusiano mzuri wa pande mbili kati ya Tehran na Lusaka.

Tovuti ya Daily Mail ya Zambia imemnukuu Rais Lungu akiyasema hayo jana Jumanne baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran mjini Lusaka, Ahmad Erfanian na kuongeza kuwa, Zambia inapendezwa na namna uchumi wa Iran ulivyostawi kwa kiasi kikubwa na nafasi ya taifa hilo duniani katika uga wa kuzalisha kwa wingi mafuta na gesi.

Amesema Zambia na Iran zina historia ya jadi ya kuwa na uhusiano na ushirikiano wa kipekee hususan chini ya mwavuli wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ya Kiafrika ina matumaini kuwa mahusiano hayo yatazidi kuimarika.

Bendera za Iran na Zambia

Kwa upande wake, Ahmad Erfanian, Balozi wa Iran mjini Lusaka amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuipa Zambia uzoefu wake katika nyuga za sayansi, tiba na kilimo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran ambaye alichaguliwa kuongoza tena taifa kwa muhula wa pili mwezi Mei mwaka huu amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, taifa hili lina hamu kubwa ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika katika nyuga mbalimbali na kwamba sera za kigeni za taifa hili zinatoa kipaumbele kwa suala hilo.