Wapinzani nchini Sudan wailaumu vikali serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33886-wapinzani_nchini_sudan_wailaumu_vikali_serikali
Mkuu wa chama cha National Umma Party cha Sudan amezikosoa vikali siasa za masuala ya kigeni za serikali ya Rais Omar al Bashir na kusema kuwa zimeigeuza Sudan kuwa kibaraka wa nchi nyingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 02, 2017 11:16 UTC
  • Sadiq al Mahdi,  Mkuu wa chama cha National Umma Party cha Sudan
    Sadiq al Mahdi, Mkuu wa chama cha National Umma Party cha Sudan

Mkuu wa chama cha National Umma Party cha Sudan amezikosoa vikali siasa za masuala ya kigeni za serikali ya Rais Omar al Bashir na kusema kuwa zimeigeuza Sudan kuwa kibaraka wa nchi nyingine.

Mtandao wa habari wa Tribune umemnukuu Sadiq al Mahdi mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Sudan akisema kuwa, serikali ya nchi hiyo imekuwa kibaraka wa kusikiliza na kutekeleza siasa za nchi nyingine kimataifa na inatafuta rizki kupitia kuingilia masuala ya nchi nyingine.

Sadiq al Mahdi ameongeza kuwa, hatua ya serikali ya Rais Omar al Bashir ya kushirikiana na Saudia katika mashambulizi dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Yemen inakinzana kikamilifu na historia ya siasa za kigeni za Sudan.

Rais Omar al Bashir wa Sudan ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imetoa waranti wa kukamatwa kwa madai ya kuhusika katika jinai za Darfur

 

Mkuu wa chama cha National Umma Party cha Sudan amesema kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, Iran ni nchi ambayo ina nafasi muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu na eneo zima la Mashariki ya Kati na kwamba Sudan inapaswa kuwa na uhusiano wa kidugu na ndugu zao wa Iran.

Anasema ni kwa manufaa ya Waislamu wote kuweko uhusiano mzuri baina ya Iran na nchi za Kiarabu na baina ya Waislamu wa Kisunni na Kishia.

Sadiq al Mahdi aidha amesema, jaribio la serikali ya Sudan la kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kosa jingine kubwa kwani linadharau uhakika kwamba ugomvi uliopo baina ya wananchi wa Sudan na utawala wa Kizayuni ni ugomvi wa kimsingi na wa dhati ambao umeshikamana barabara na wajibu wa utawala wa Kizayuni kuwarejeshea Wapalestina haki zao zote.