Jeshi la Sudan lakanusha kushambulia waasi katika jimbo la Blue Nile
Jeshi la Sudan limekanusha kushambulia eneo la waasi katika jimbo la Blue Nile.
Jeshi la Sudan limetoa taarifa na kusisitiza ahadi zake za kusitisha mapigano katika maeneo yote ya migogoro, na kukanusha madai ya waasi kwamba jeshi hilo lilishambulia eneo lao katika jimbo la Blue Nile.
Siku ya Ijumaa, kundi la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan (SPLM) – Eneo la Kaskazini- lilishutumu jeshi la serikali ya Khartoum kuwa limeshambulia ngome yake katika jimbo hilo.
Msemaji wa jeshi la Sudan Ahmed Khalifa Al-Shami ameeleza kuwa, jeshi la Sudan linasisitiza tena ahadi zake za kusitisha mapigano dhidi ya waasi.
Amesema shutuma ya waasi ina kusudi la kuharibu ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Sudan huko Washington.
Mwezi Julai, Rais wa Sudan Omar al-Bashir alitangaza kusimamisha mapigano katika maeneo yote ya migogoro kwa miezi mitatu hadi Oktoba mwaka huu.