Watu 50 wauawa, 50,000 wakimbia mapigano mashariki mwa Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34541-watu_50_wauawa_50_000_wakimbia_mapigano_mashariki_mwa_ethiopia
Watu zaidi ya 50 wameuawa katika mapigano ya wiki moja katika maeneo la Oromiya na Somali nchini Ethiopia huku wengine 50,000 wakilazimika kukimbia makazi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2017 22:08 UTC
  • Watu 50 wauawa, 50,000 wakimbia mapigano mashariki mwa Ethiopia

Watu zaidi ya 50 wameuawa katika mapigano ya wiki moja katika maeneo la Oromiya na Somali nchini Ethiopia huku wengine 50,000 wakilazimika kukimbia makazi yao.

Wakazi wa maeneo hayo mawili wanarushiana lawama kuhusu chanzo cha kuibuka machafuko hayo. Mkuu wa mkoa wa Oromiya Lema Megersa amesema serikali itawachukulia hatua wahusika wa machafuko hayo.

Baadhi ya maafisa wa Oromiya wanasema mapigano hayo yalianza baada ya mkuu mmoja wa wilaya kuuawa wakati wa hujuma ya wanamgambo kutoka eneo la Somali (Ogaden). Hata hivyo maafisa wa eneo la Somali wamekanusha madai hayo na kusema watu 50 wa jamii ya Somali waliuawa Jumanne katika mji wa Aweday katika eneo la Oromiya.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Eneo hilo la mashariki mwa Ethiopia limekuwa likikumbwa na mapigano ya mara kwa mara ambapo katika machafuko ya mwaka 2015 na 2016 huko Oromiya na baadhi ya maeneo mengine ya karibu, watu 669 waliuawa.

Siku ya Jumapili Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alitangaza kutuma wanajeshi katika eneo la mapigano kwa lengo la kuwapokonya silaha wanamgambo na kulinda barabara muhimu katika eneo hilo. Taarifa zinasema tayari mamia ya watu wanaoshukiwa kuhusika na mapigano hayo wameshakamatwa.