Sudan yaitaka Marekani iondoe vikwazo dhidi yake
Rais wa Sudan ametaka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi yake.
Rais Omar al Bashir wa Sudan amesema kuwa Marekani inapasa iiondolee nchi yake vikwazo kwa kuzingatia hatua ya Washington ya kukiri kwamba Khartoum imeheshimu na kufungamana na ahadi zake zote. Rais wa Sudan ameyasema hayo alipokutana na kuzungumza na wataalamu pamoja na wanaharakati wa masuala ya habari wa Marekani.
Licha ya Sudan kusisitiza kuwa imepiga hatua katika masuala matano iliyofikia kati yake na serikali ya Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama kwa ajili ya kuondoa vikwazo vinavyoikabili, lakini Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kwa upande wake imesema kuwa kuondolewa vikwazo hivyo kutategemea rekodi ya haki za binadamu ya Sudan. Mwezi Januari uliopita Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama aliagiza kuondolewa vikwazo dhidi ya Sudan na dikrii hiyo ilitazamiwa kutekelezwa mwezi Juni kwa lengo la kuishawishi serikali ya Sudan kuendeleza jitihada zake kuhusu masuala ya haki za binadamu na mapambano dhidi ya ugaidi.
Khartoum inataraji kuwa vikwazo ilivyowekewa na Marekani tangu mwaka 1997, vitaondolewa mwezi Oktoba mwaka huu.