Wanafunzi 6 na mlinzi wauawa baada ya shule kuvamiwa na maharamia Kenya
Kwa akali wanafunzi sita na bawabu wa shule moja katika mji wa Lokichogio, kaskazini mwa Kenya wameuawa baada ya shule yao kuvamiwa na maharamia wanaoaminika kutoka Sudan Kusini, usiku wa kuamkia leo.
Gavana wa kaunti ya Turkana, Josphat Nanok amethibitisha kutokea uvamizi huo sambamba na kulaani hujuma hiyo dhidi ya wanafunzi wasio na hatia.
Kamishna wa kaunti ya Turkana, Seif Matata amethibitisha kutokea mauaji hayo na kubainisha kuwa, mmoja wavamizi hao alikuwa mwanafunzi wa shule hiyo, ambaye alikuwa amefukuzwa shuleni kutokana na utovu wa nidhamu.
Habari zinasema kuwa, maharamia hao wamevamia Shule ya Sekondari ya AIC Lokichogia katika kaunti ya Turkana na kutekeleza unyama huo.
Habari zaidi zinasema kuwa, baadhi ya mabinti wa shule hiyo wamebakwa katika tukio hilo la jana usiku.
Waliopata majeraha madogo wamelazwa katika Hospitali ya Lopiding huku wenye majeraha madogo wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Lodwar Kaunti ya Turkana.