Magaidi wavunja benki na kushambulia kanisa Misri, 7 wauawa
Kwa akali watu saba wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya genge moja la kigaidi kuvamia benki na kuiba, sambamba na kushambulia kanisa katika eneo la Sinai, kaskazini mwa nchi.
Shirika la habari la AP limeripoti kuwa, genge hilo mapema leo limeingia katika mji wa Arish na kisha kugawanyika katika vijikundi viwili. Kundi moja limevamia Kanisa la Saint George kwa maguruneti.
Genge la pili limeripotiwa kuvamia benki moja karibu na kanisa hilo, ambapo limerusha maguruneti na kisha kukabiliana kwa risasi na walinzi wa benki hiyo.
Watu saba wakiwemo raia watatu wameuawa katika mashambulizi hayo ya leo Jumatatu katika eneo la Sinai ambalo limekuwa likishuhudia mapigano kati ya maafisa usalama na magenge ya kigaidi yenye mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Aidha watu 15 wakiwemo watoto wadogo na wanawake wamejeruhiwa katika hujuma hizo za kigaidi.
Ashraf Hanafi, mwalimu katika mji wa Arish ambaye ameshuhudia matukio hayo amesema milio ya risasi imesikika kwa takriban masaa mawili.
Hii ni katika hali ambayo, jeshi la Misri limetangaza habari ya kuua wanachama 24 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika mji wa Sheikh Zweid katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa nchi.
Kadhalika wanajeshi sita wa Misri wameuawa huku wengine 20 wakijeruhiwa katika makabiliano hayo ya jana Jumapili.