Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asisitiza kutumwa askari zaidi CAR
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kutumwa askari 900 wa kofia buluu wa umoja huo kwa ajili ya kusimamia amani Jamhuri ya Afrika ya Kati.
António Guterres amesema hayo katika ripoti yake iliyotangazwa jana na kuongeza kuwa, kwa kuzingatia kwamba kumezuka wimbi jipya la machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, inabidi askari wengine 900 wa kofia buluu watumwe nchini humo chini ya mwavuli wa kikosi cha MINUSCA.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, hali ya usalama imezidi kuwa mbaya katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni hususan kwenye eneo la kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, jambo ambalo linachochea kuzuka wimbi jipya la machafuko nchini humo.
Itakumbukwa kuwa muda wa kuhudumu kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kusimamia amani Jamhuri ya Afrika ya Kati kinamalizika mwezi ujao wa Novemba 2017.
Kikosi hicho cha MINUSCA kinaundwa na wanajeshi elfu kumi na raia elfu mbili. Kilitumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2013 ili kuvisaidia vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kulinda amani.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia kwenye machafuko makubwa ya kisiasa mwaka 2013 kutokana na uchochezi wa nchi za Magharibi. Maelfu ya watu hasa Waislamu wameuawa na kujeruhiwa na mamia ya maelfu ya wengine wamekuwa wakimbizi hadi hivi sasa.