Misri yakataa kuburuzwa na Saudia; yapinga vikwazo dhidi ya Hizbullah ya Lebanon
-
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri (kushoto) na Mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amesisitiza kuwa, licha ya Saudi Arabia kuzitaka nchi za Kiarabu ziiwekee vikwazo Hizbullah ya Lebanon lakini Cairo haina nia kabisa ya kufanya hivyo.
Shirika la habari la Mehr limemnukuu el Sisi akisema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya CNBC ya Marekani na kubainisha kwamba, eneo Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika limetumbukia kwenye hali mbaya kutokana na machafuko ya Syria, Iraq, Yemen na Libya hivyo si sawa kulibebesha matatizo mengine eneo hili.
Itakumbukwa kuwa Saudia ni moja ya waitifaki wa Misri. Viongozi wa Saudia wanadai kuwa lazima Hizbullah ya Lebanon ipokonywe silaha na isishirikishwe katika serikali ya nchi hiyo. Vile vile baada ya waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri kutangaza ghafla kujiuzulu tena akiwa nchini Saudia, Riyadh imeongeza njama za kuisakama Hizbullah ya Lebanon na kudai eti ni hatari kwa nchi hiyo ikiwa ni uingiliaji wa wazi wa masuala yasiyoihusu ya ndani ya Lebanon.
Itakumbukwa kuwa Hizbullah ya Lebanoni imekuwa ikiendesha mapambano yake dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni tu na haijawahi kutishia usalama wa nchi yoyote ya Kiarabu. Iran na Hizbullah ya Lebanon ziko mstari wa mbele katika kukabiliana na njama za Wazayuni zinazotekelezwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kuzitumia baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Saudi Arabia kuzifanikisha.
Hizbullah ya Lebanon inaiambia Saudi Arabia kwamba harakati hiyo haijawahi hata kuomba msaada wa Saudia na haijawahi na wala haina nia kabisa ya kutishia usalama wake, sasa ni kitu gani kinawafanya viongozi wa Saudia kuifanyia uadui harakati hiyo ya Kiislamu, au ni kwa kuwa imesimama kidete kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel?