MDC: Kuuita uwanja wa ndege wa kimataifa "Mugabe" ni tusi kwa Wazimbabwe
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC kimekosoa vikali hatua ya kubadilisha jina la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harare na kuuita Robert Gabriel Mugabe, jina la rais wa nchi hiyo.
Msemaji wa chama hicho, Obert Gutu amesema ni tusi kubwa na dhihaka kwa Wazimbabwe wa matabaka yote kubadilishwa jina la uwanja huo kutoka Harare na kuitwa Robert Gabriel Mugabe.
Amesema jina la uwanja huo wa ndege litarejeshwa kuwa Harare mwaka ujao wakati ambapo chama hicho kitaingia madarakani kikishinda uchaguzi wa rais.
Msemaji huyo wa chama cha MDC amesema kiongozi huyo mkongwe wa Zimbabwe ameigeuza jamhuri hiyo kuwa milki yake binafsi, kwani tayari barabara na majengo mengi ya kiserikali kama vyuo vikuu yamepachikwa jina lake.
Siku ya Alkhamisi, Wizara ya Uchukuzi ya Zimbabwe ilifanya sherehe za kulibadili jina la uwanja huo wa ndege, kwa heshima ya rais wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 93.
Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe amesema siku za Mugabe kuwa madarakani zinahesabika, na karibuni hivi wananchi watanyakua uhuru na hadhi yao kutoka kwenye makucha ya rais huyo na vibaraka wake walio mafisadi serikalini.