Mapinduzi ya Zimbabwe; maji yamfika shingoni Mugabe, ajiandaa kujiuzulu
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anajiandaa kuondoka madarakani saa chache baada ya jeshi la nchi hiyo kutwaa madaraka kwa njia isiyo ya umwagaji damu.
Meja Jenerali SB Moyo, Mkuu wa Jeshi la Zimbabwe ametangaza kwenye kituo cha runinga cha serikali ZBC baada ya jeshi kukidhibiti kuwa, hatua yao ya kutwaa madaraka inalenga wahalifu na kwamba Mugabe na familia yake wako salama.
Habari zinasema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wametapakaa katika barabara zote muhimu za mji mkuu Harare, na hususan zinazoelekea katika majengo ya serikali, Bunge na mahakama.
Wakati huo huo, chama kikuu cha upinzani nchini humo cha MDC kimetoa wito wa kurejea katika mfumo wa demokrasia kwa njia za amani.
Chama tawala nchini Zimbabwe, Zanu PF kimemtuhumu Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo kuwa amekiuka katiba kwa kutishia kuingilia kati mgogoro wa nchi hiyo baada ya Rais Robert Mugabe kuitumbukiza nchi katika mgogoro kwa kumtimua makamu wake aliyekuwa na ushawishi mkubwa, Emmerson Mnangagwa wiki iliyopita.
Jioni ya jana kuliripotiwa kuzingirwa jengo la televisheni ya taifa ya ABS na jeshi, huku jeshi jeshi hilo likitangaza kwamba hatua hiyo ilichukuliwa kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi wa jengo hilo.