Mnangagwa aapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe, aahidi kulijenga upya taifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36747-mnangagwa_aapishwa_kuwa_rais_mpya_wa_zimbabwe_aahidi_kulijenga_upya_taifa
Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na Robert Mugabe wiki chache zilizopita ameapishwa hii leo kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, huku akiahidi kulijenga upya taifa hilo linalokabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2017 12:28 UTC
  • Mnangagwa aapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe, aahidi kulijenga upya taifa

Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na Robert Mugabe wiki chache zilizopita ameapishwa hii leo kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, huku akiahidi kulijenga upya taifa hilo linalokabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.

Sherehe za kumuapisha Mnangagwa zimefanyika katika Uwanja wa Taifa wa Michezo mjini Harare, uliokuwa umefurika makumi ya maelfu ya wananchi wanaosema kuwa nchi yao inashuhudia mwamko mpya.

Katika hotuba yake ya dakika 30 hivi kwa taifa, Mnangagwa ambaye anafahamika kwa jina la kimajazi kama "Mamba" ameahidi kushirikiana na wadau wote katika kuliongoza taifa akisisitiza kuwa atakuwa kiongozi wa wananchi wa matabaka yote.

Chini ya sauti za kumshangilia zilizohinikiza uwanjani hapo, kiongozi huyo amesema: "Sauti ya wananchi ni sauti ya Mungu. Nitalitumikia taifa zima pasina kumbagua yeyote katika misingi ya rangi, dini, kabila au mrengo wake wa kisiasa."

Mugabe hakuhudhuria sherehe za kuapishwa Mnangagwa

Amezitaka nchi za Magharibi kuiondolea nchi hiyo vikwazo vya uchumi, huku akibainisha kuwa, serikali yake itazingatia utawala wa sheria na demokrasia.

Mbali na kuwataka Wazimbabwe kuwa na utamaduni wa kusameheana na kuvumiliana, ameahidi kubuni nafasi za ajira, katika taifa hilo ambalo limeshuhudia raia wake zaidi ya milioni 3 wakikimbilia nchi jirani ya Afrika Kusini kutafuta ajira.

Kadhalika ameahidi kwamba mtangulizi wake, Robert Mugabe ataendelea kutambulia kama shujaa wa kupigania uhuru, na kubainisha kwamba mwanasiasa huyo mkongwe atapewa kinga ya kutoshtakiwa na kupewa usalama wa kutosha yeye na familia yake.

Mugabe na mkewe Grace. 

Jumanne iliyopita, Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 37 alisalimu amri na kukubali kujiuzulu, kufutia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.

Emmerson Mnangagwa ataiongoza Zimbabwe hadi Septemba mwaka ujao 2018, wakati ambapo uchaguzi wa rais utafanyika.