Mugabe alidondokwa na machozi na kukubali shingo upande kuachia madaraka
Gazeti la Standard linalochapishwa nchini Zimbabwe limefichua kuwa, aliyekuwa rais wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, Robert Mugabe alionekana akilia huku akisema 'usaliti' wakati alipokubali kuachia madaraka kufuatia mashinikizo ya kila upande wiki iliyopita.
Chapisho la leo Jumapili la gazeti hilo binafsi limenukuu duru za habari zilizoshuhudia mazungumzo yaliyopeleka Mugabe kukubali kujiuzulu zikisema kuwa, wakati wa mazungumzo hayo, kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93 aliinamisha kichwa chini huku akisema 'Wanadamu ni vinyonga'.
Hata hivyo gazeti la serikali la Sunday Mail limemnukuu Fidelis Mukonori, Padri wa Kanisa Katoliki aliyeongoza mazungumzo kati ya Mugabe na Jeshi la nchi hiyo akisema kuwa, "Uso wake (Mugabe) uling'ara kwa bashasha baada ya kusaini barua ya kukubali kujiuzulu. Sidhani kama alikuwa na machungu moyoni. Binafsi nilimfahamisha kwamba kujiuzulu kwake ni kwa maslahi yake mwenyewe na kwamba ni vyema atizame mtu mwingine akiiongoza nchi."
Jumanne iliyopita, Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 37 alisalimu amri na kukubali kujiuzulu, kupitia barua aliyomtumia Spika wa Bunge la nchi hiyo.
Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na Robert Mugabe wiki chache zilizopita na kwenda uhamishoni Afrika Kusini aliapishwa Ijumaa iliyopita mjini Harare kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Alisema Mugabe ataendelea kutambulia kama shujaa mpigania uhuru, na kubainisha kwamba mwanasiasa huyo mkongwe atapewa kinga ya kutoshtakiwa mbali na kupewa usalama wa kutosha yeye na familia yake.