Mnangagwa ateua baraza la mawaziri, wanajeshi na wapambe wa Zanu-PF wafaidi
Emmerson Mnangagwa, Rais mpya wa Zimbabwe ameteuwa baraza lake jipya la mawaziri, linalojumuisha maafisa wa ngazi za juu kwenye jeshi la nchi hiyo na viongozi 'waaminifu' wa chama tawala ZANU-PF.
Baraza hilo la mawaziri 22 hata hivyo halina shakhsia na wanasiasa wa upinzani. Katika taarifa iliyorushwa hewani na televisheni ya serikali jana jioni, Mnangagwa amemteua Meja Jenerali Sibusiso Moyo, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, kamanda wa jeshi la anga, Perrance Shiri kuwa Waziri wa Kilimo, na Chris Mutsvangwa, kiongozi wa Muungano wa Maveterani ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari miongoni mwa wengine.
Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, kiongozi wa upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai amesema Mnangagwa ana 'kidirisha kidogo' cha kuonyesha kuwa yuko tofauti na Mugabe na kutimiza matarajio ya wananchi walio wengi. Amesema hadi sasa hayajaitishwa mazungumzo yoyote baina yao na 'uongozi mpya' wa taifa hilo.
Awali chama cha upinzani cha MDC kilitaka kuundwa serikali jumuishi ya mpito ili kuhitimisha utawala wa miaka 37 wa Mugabe na kuruhusu mageuzi kwa ajili ya kufanyika uchaguzi halali na huru mwaka ujao huko Zimbabwe.
Emmerson Mnangagwa aliapishwa kuwa Rais Mpya wa Zimbabwe Ijumaa iliyopita baada ya Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93 kujiuzulu kiti cha urais kwa kushinikizwa na jeshi na chama chake.
Baada ya kuapishwa, aliahidi kufufua uchumi wa nchi hiyo uliozorota na kuwahudumia raia wote wa nchi hiyo bila ya kubagua.